Maskani ya Vitabu na Maarifa
🎯 Vitabu
🎯 Maarifa
🎯 Maendeleo binafsi
17/10/2026
KANUNI YA 19: NI VIGUMU ZAIDI KUJITAWALA KULIKO ILIVYO KUSIMAMIA FEDHA ZAKO
Namna Tunavyojifahamu.
Mara nyingi, tunadhani tunajifahamu vizuri kwa sababu tunajua tunachotaka kufikia na mambo tunayoyaamini kuwa tunaweza au hatuwezi kuyafanya.
Hata hivyo, kujifahamu kwa kina kunahitaji kuelewa tabia zetu tunapokabiliwa na changamoto, vishawishi na majukumu yanayohitaji uvumilivu.
Watu wengi huweka azma ya kubadilisha maisha yao. Mtu anaweza kuamua kupunguza uzito, kuimarisha utimamu wa mwili, kuanzisha biashara, kuweka akiba au kujenga utajiri. Mwanzoni, huwa na hamasa kubwa, lakini kadiri muda unavyopita, changamoto zinapoongezeka na matokeo yanapochelewa, wengi hushindwa kuendelea.
Hali hii inatufundisha kuwa kujua tunachotaka si sawa na kuwa na nidhamu ya kufanya kile kinachohitajika ili kukipata.
Kujifahamu kunahitaji kutambua uwezo wetu, udhaifu wetu na tabia zinazotusaidia au kutukwamisha. Kutambua ni hatua muhimu inayowezesha kufanyia kazi tunavyojitambua.
Uwezo Uliojificha na Umuhimu wa Kujitawala.
Wakati mwingine, hatujui uwezo tulio nao mpaka tunapokutana na mazingira yanayotulazimisha kuutumia. Mtu anaweza kuamini kuwa hawezi kufanya maamuzi magumu, kutatua matatizo au kuishi bila utegemezi fulani. Lakini anapojikuta hana msaada na hana chaguo jingine, hulazimika kufikiri, kujifunza na kuchukua hatua. Katika mchakato huo, anaweza kugundua ujasiri, uvumilivu na uwezo ambao hakujua anao.
Hata hivyo, hatupaswi kusubiri mazingira yatulazimishe ndipo tugundue uwezo wetu. Tunaweza kujaribu kwa hiari mambo na hali ambazo tunadhani hatuwezi, kukubali majukumu mapya, kufanya mambo magumu ambayo tumekuwa tukiyaahirisha. Kwa kufanya hivyo, tunakuwa tunajifunza kuhusu uwezo wetu na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
Hapa ndipo dhana ya kujitawala inapokuwa muhimu. Kujitawala ni uwezo wa kudhibiti matamanio, hisia na tabia zetu ili kufanya kile kinachohitajika badala ya kutawaliwa na msukumo wa muda mfupi. Kunahusisha nidhamu, uvumilivu, na kufanya maamuzi yanayozingatia malengo ya muda mrefu.
Kujitawala ndio msingi wa kusimamia fedha binafsi, huwezi kuwa na usimamizi wa fedha zako ikiwa hujajenga kwanza uwezo wa kujitawala.
Kwahiyo urahisi au ugumu katika kusimamia fedha zako, upo katika kujitawala.
Kujitawala kunatoa nafasi ya kusimamia fedha kwa sababu kunatusaidia kufuata bajeti, kuweka akiba, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuepuka maamuzi ya kifedha yanayotokana na papara, wivu au shinikizo la jamii. Hata hivyo, nidhamu inapaswa kuambatana na maarifa ya fedha na mipango inayozingatia kipato na mahitaji halisi ya mtu.
Hata hivyo, kujitawala hakumaanishi kuishi maisha ya mateso au kujinyima kila kitu. Kunamaanisha kufanya maamuzi kwa kuzingatia vipaumbele vyako badala ya kutawaliwa na hisia za muda mfupi. Fedha zinapaswa kutumika kuboresha maisha, lakini matumizi ya leo hayapaswi kuharibu uwezo wako wa kujenga maisha bora ya kesho.
Hatua za vitendo za kutekeleza kanuni hii
1. Jifunze kujitambua. Tambua tabia zinazokwamisha maendeleo yako ya kifedha, kisha fanyia kazi tabia moja kwa moja kwa kuijengea tabia chanya mbadala.
2. Weka mifumo inayokusaidia kujitawala. Badala ya kutegemea dhamira pekee, weka mazingira ya mfumo inayokusaidia mf. Mtu wa kuwajibika kwake, kukatwa akiba moja kwa moja n.k
3. Jifunze kutathmini na kujisubirisha kwenye maamuzi ya fedha. Kabla ya kufanya matumizi yasiyo ya lazima, jiulize k**a fedha hizo pana ulazima zitumike hivyo, na jipe muda zaidi ili kujua k**a ni hitaji la muhimu ama ni msukumo wa kihisia tu.
4. Jenga uvumilivu. Kubali kuwa biashara, uwekezaji na ukwasi huhitaji muda, maarifa na juhudi endelevu, si kitu cha usiku mmoja.
5. Fuatilia maendeleo yako. Kagua matumizi, akiba na hatua ulizopiga kila wiki au kila mwezi ili kujua k**a tabia zako zinakupeleka karibu na malengo yako.
Unaweza kupata kipato kikubwa na bado usijenge ukwasi ikiwa huna nidhamu ya matumizi. Vivyo hivyo, unaweza kuanza na kipato kidogo lakini ukajenga msingi mzuri wa ukwasi kwa kujifunza, kuweka akiba, kuwekeza na kufanya maamuzi yenye busara.
Kwa sababu mara nyingi, kikwazo kikubwa kati ya mtu na malengo yake ya kifedha si fedha, kwa sababu fedha karibu kila mtu anapata, bali ni tabia anazoshindwa kuzidhibiti.
Kujenga ukwasi kunahitaji uwezo wa kupata fedha, lakini pia uwezo wa kujitawala unapozipata. Kabla ya kutaka kusimamia fedha nyingi, jifunze kwanza kujitawala, simamia tabia na maamuzi yanayoathiri matumizi yako.
Karibu kundini;
https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?s=cl&p=a&mlu=0
16/10/2026
KANUNI YA 18: USIWAONEE WENGINE WIVU KWA KILE WALICHO NACHO
Kila mtu ana malengo yake, matamanio yake na kiwango cha juhudi alicho tayari kutoa ili kufikia mafanikio. Pia, kila mtu ana mipaka yake kuhusu mambo anayoweza kufanya na yale ambayo hayuko tayari kuyafanya linapokuja swala la la mafanikio.
Kwa hiyo, kuwaonea wengine wivu kwa sababu ya utajiri walio nao si jambo lenye manufaa, hasa pale ambapo hujui safari yao ilikuwaje, walifanya kazi kiasi gani, walijifunza nini au walijitoa kwa kiasi gani ili kufikia walipo.
Wakati mwingine unaona mtu anaishi maisha ya kifahari, ana biashara kubwa au ana fedha nyingi, kisha unatamani kuwa k**a yeye. Lakini unachokiona ni matokeo, si historia nzima iliyosababisha matokeo hayo.
Huenda mtu huyo alifanya kazi na malengo kwa miaka mingi, alijifunza ujuzi maalumu, alianzisha biashara iliyomgharimu mambo mengi kuifanikisha, alichukua hatua ambazo wengine hawakuwa tayari kuzichukua na alijinidhamisha kwenye mambo ambayo wengine hawako tayari.
Richard Templar anasisitiza kuwa kuwaonea matajiri wivu hakutufanyi kuwa matajiri, lakini kujifunza kutoka kwao kunaweza kutuonyesha njia ya kufikia mafanikio.
Unapokutana na mtu aliyefanikiwa kifedha, unapaswa kuuliza alianzaje, alitumia mbinu gani, alikabiliana vipi na changamoto na ni mambo gani unaweza kujifunza kutoka kwake.
Mwandishi pia anasisitiza umuhimu wa kuwa na mwanasihi wa maswala ya fedha, yaani mtu mwenye uzoefu wa kifedha ambaye unaweza kujifunza kutoka kwake.
Mshauri wa aina hii anaweza kukusaidia kuelewa namna ya kutengeneza fedha, kuzisimamia, kuwekeza na kujenga utajiri wa muda mrefu.
Na si sahihi kutegemea tu ushauri wake, bali pia kuchunguza matokeo ya mbinu zake na kujifunza namna ya kuzitumia katika mazingira yako.
Hata hivyo, kujifunza kutoka kwa wengine hakumaanishi kuiga kila wanachofanya. Kila mtu ana mazingira, uwezo, fursa na changamoto zake. Njia iliyomfaa mtu mmoja huenda isifae mwingine. Jambo la msingi ni kuelewa kanuni zilizoleta mafanikio, kisha kuzitumia kwa namna inayolingana na hali yako.
Kwa upande mwingine, wivu unaweza kutufanya tutumie muda mwingi kufuatilia mafanikio ya wengine badala ya kujenga yetu wenyewe. Tunaweza kuanza kudharau maendeleo yetu kwa sababu tunajilinganisha na watu ambao wamekuwa kwenye safari ya mafanikio kwa muda mrefu zaidi. Matokeo yake, tunapoteza umakini, tunafanya maamuzi kwa pupa au tunaanza kutamani mafanikio bila kuwa tayari kufanya kazi inayohitajika.
Ujumbe mkuu wa kanuni hii ni kwamba mafanikio ya wengine yanapaswa kuwa chanzo cha hamasa na kujifunza, si sababu ya kujiona tumeshindwa.
Kumbuka: Hatuhitaji kuwashinda wengine ili tufanikiwe. Tunahitaji kuelewa malengo yetu, kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa na kufanya kazi kwa nidhamu ili kufikia tulipojipangia.
Kuwaonea wengine wivu hakuna faida; kujifunza kutoka kwao kuna thamani kubwa.
15/10/2026
KANUNI YA 17: ELEWA NAMNA MATAJIRI WANAVYOFIKIRI
Fahamu zako na fikra zako zimejengwa katika nini?
Katika ulimwengu wa leo, unaweza kupata picha ya mambo yanayovutia akili ya mtu kwa kuangalia namna anavyotumia mitandao ya kijamii. Angalia aina ya maudhui anayoyatazama zaidi, akaunti anazozifuatilia na muda anaotumia kujifunza kupitia mitandao hiyo.
Mitandao ya kijamii hutumia mifumo ya kanuni za algoriti (algorithm) kuchagua na kupendekeza maudhui yanayoweza kumvutia mtumiaji. Kadiri unavyotazama, kupenda, kutoa maoni au kushiriki maudhui ya aina fulani, ndivyo unavyoweza kuendelea kuonyeshwa maudhui yanayofanana nayo.
Kwa hiyo, unaweza kuona katika muda anaotumia kwenye mitandao ya kijamii, akili yake inajazwa na nini zaidi.
K**a anatumia muda mwingi kufuatilia udaku, migogoro ya watu maarufu, mpira, vichekesho, maisha ya watu wengine, na burudani nyingine huyo ufikiri wake umejengwa, unajengwa na kupevuka katika hivyo.
K**a anatumia sehemu ya muda huo kujifunza kuhusu biashara, uwekezaji, usimamizi wa fedha, uzoefu wa watu waliofanikiwa kujenga ukwasi, elimu ya kiroho na namna inavyohusiana na ukwasi, huyo fikira zake zinajengwa hivyo.
Nimetolea mfano wa matumizi ya mitandao ya kijamii kueleza picha ya fikra za mtu lakini pia pana mifano mingine inayoweza kuonesha nini kinatawala fikra za mtu.
Kile unachokipa umakini mara kwa mara kinaweza kuathiri mambo unayoyajua, namna unavyofikiri na maamuzi unayofanya.
CHAGUA UNACHOLISHA AKILI YAKO
Mtu anayetaka kujenga ukwasi anapaswa kujifunza namna watu wenye ukwasi wanavyofikiri na kufanya maamuzi.
Maana yake ni kwamba, ikiwa una lengo la kujenga ukwasi, unapaswa kutafuta maarifa yanayoweza kukusogeza karibu na lengo hilo katika fikra kwanza.
Unaweza kufuatilia maudhui yanayokufundisha namna ya kuanzisha biashara, kutambua fursa, kusimamia mapato, kuweka akiba, kuwekeza na kujenga vyanzo vya mapato.
Unaweza kufuatilia wajasiriamali wenye uzoefu, wawekezaji, wachambuzi wa biashara na watu wanaofundisha elimu ya fedha. Sikiliza mahojiano yao, soma vitabu wanavyopendekeza na chunguza maamuzi yaliyowasaidia kufanikiwa.
Unapogeuza fikra zako kuwa k**a za matajiri kwa kujifunza kuhusu ukwasi, unakuwa umejisogeza na asili hiyo, kinachobaki inakuwa ni kuweka kwenye vitendo unachojifunza.
JIFUNZE NAMNA WATU WENYE UKWASI WANAVYOFIKIRI
Richard Templar anasisitiza umuhimu wa kujifunza kuhusu fedha ikiwa unataka kuongeza ukwasi wako. Hii inahusisha kuelewa namna watu wanavyopata fedha, kuzisimamia, kuzihifadhi na kuzifanya zizae thamani zaidi.
Usijifunze tu kuhusu kiasi cha fedha walicho nacho (networth) watu waliofanikiwa. Jifunze kuhusu mifumo yao ya kufikiri, nidhamu yao, namna wanavyotathmini hatari, maamuzi yao ya uwekezaji na makosa waliyofanya njiani.
Jiulize maswali k**a haya:
- Ni maarifa gani ninayohitaji ili kuboresha hali yangu ya kifedha?
- Ni tabia zipi zinazonipotezea muda bila kuniongezea maarifa au thamani?
- Ni watu gani ninaoweza kujifunza kutoka kwao?
- Ni jambo gani nililojifunza leo ambalo ninaweza kulitekeleza katika maisha yangu?
Maswali haya yanaweza kukusaidia kuhamisha umakini wako kutoka kwenye kutazama mafanikio ya watu wengine kwenda kwenye kujenga mafanikio yako mwenyewe.
MAFUNZO MUHIMU YA KANUNI HII
1. Linda umakini wako: Muda unaoutumia kila siku una thamani. Usiuache uelekezwe kwenye maudhui na mambo yasiyojenga ufikiri wako.
2. Jifunze kuhusu fedha: Fuatilia elimu ya biashara, akiba, uwekezaji na usimamizi wa fedha.
3. Geuza maarifa kuwa vitendo: Tumia unachojifunza kuboresha maamuzi na kujenga mifumo yako ya kifedha.
4. Jifunze kwa mwendelezo: Ukwasi unahitaji maarifa, nidhamu, maamuzi yenye busara na utekelezaji wa muda mrefu, hivyo jiongezee maarifa kila siku, ni kwa namna hiyo tu ndo unaweza kufika mbali. Siku zote unapoacha kujifunza unaacha kukua na pia kasi yako ya kujifunza ndio kasi yako ya ukuaji.
14/10/2026
KANUNI YA 16: ELEWA TOFAUTI KATI YA GHARAMA NA THAMANI
Richard Templar anasisitiza umuhimu wa kuelewa tofauti kati ya gharama na thamani. Anaeleza kuwa vitu havipaswi kupimwa kwa kiasi cha fedha kilicholipwa pekee, kwa sababu thamani yake inaweza kuwa kubwa au ndogo kuliko gharama yake kulingana na manufaa, mazingira na namna vinavyotazamwa.
Anasimulia jinsi alivyowahi kumuuliza baba mkwe wake kuhusu mvinyo unaouzwa kwa 35,0000 (TZS) katika mgahawa wa kifahari. Je, kweli mvinyo huo unaweza kuwa bora mara 20 kuliko mvinyo unaouzwa kwa 17,500 (TZS) katika duka la kawaida?
Jibu la baba mkwe wake lilikuwa la kuvutia. Alieleza kuwa unapolipia mvinyo katika mgahawa wa kifahari, hulipii mvinyo pekee, bali pia mazingira ya mgahawa, huduma, eneo ulipo, utaalamu wa mhudumu, faragha, ubora wa chakula, watu unaokula nao, mazungumzo mazuri na hata historia na hadhi ya mahali hapo. Kwa hiyo, mvinyo wenyewe ni sehemu ndogo tu ya kile unacholipia.
Gharama ni kiasi cha fedha kinacholipwa kupata kitu, lakini thamani ni umuhimu, manufaa au manufaa yanayotokana na kitu hicho kwa mtu anayekimiliki au kukitumia.
TUCHIMBUE KWA KINA
Kanuni hii inatufundisha kuwa tusichanganye gharama ya kupata kitu na manufaa au thamani yake halisi.
Watu wengi hufanya maamuzi ya kifedha kwa kuangalia gharama (bei) pekee, bila kujiuliza wanapata nini kutokana na fedha wanazotumia.
Kwa mfano, unaweza kununua simu kwa TSh 300,000 na nyingine ikawa inauzwa kwa TSh 600,000. Simu ya pili si lazima iwe na thamani mara mbili kwa kila mtu.
Ikiwa simu ya bei ya chini inakidhi mahitaji yako yote, wakati simu ya bei ya juu ina vipengele ambavyo hutavitumia, basi simu ya bei ya chini inaweza kuwa na thamani kubwa zaidi kwako.
Vivyo hivyo, bidhaa ya bei ya juu inaweza kuwa na thamani nzuri ikiwa inadumu kwa muda mrefu, inakupunguzia gharama za matengenezo au inakusaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Jambo hili ni muhimu zaidi tunapozungumzia ukwasi. Mtu anayejenga utajiri anapaswa kujifunza kutumia fedha kwa kuzingatia thamani anayopata, badala ya kuvutiwa na bei au mwonekano wa kitu pekee.
Pia, thamani inaweza kuwa ya aina tofauti. Kuna thamani ya matumizi, thamani ya kifedha, thamani ya kihisia na thamani inayotokana na hadhi au uzoefu.
Nyumba inaweza kuwa na thamani ya kifedha kutokana na eneo lake, lakini pia ikawa na thamani ya kihisia kwa sababu ni ya urithi yaani ni sehemu ya kumbukumbu za mahali ulipokulia, wazazi na historia ya familia.
MAFUNZO YA KIFEDHA KUTOKANA NA KANUNI HII
1. Usinunue kwa kuangalia bei pekee. Jiulize bidhaa au huduma hiyo itakusaidia nini, itadumu kwa muda gani na k**a inaendana na mahitaji yako.
2. Jifunze kutambua thamani iliyofichika. Wakati mwingine fursa nzuri za kifedha hupatikana katika vitu ambavyo watu wengine wamevipuuza kwa sababu ya mwonekano wake, umri wake au bei yake ya chini.
3. Unapouza, elewa thamani unayotoa. Katika biashara, wateja hawalipii bidhaa pekee; wanaweza pia kulipia urahisi, huduma nzuri, uaminifu, muda wanaookoa na uzoefu wanaoupata. Kadiri unavyoelewa mahitaji ya wateja wako, ndivyo unavyoweza kuboresha thamani ya bidhaa au huduma yako.
4. Tofautisha thamani unayoiona na bei ambayo soko litakubali. Unaweza kuipa mali yako thamani kubwa kutokana na sababu binafsi, lakini unapoiuza, lazima uzingatie pia mahitaji ya wanunuzi na kiasi wanachokuwa tayari kulipa.
Kumbuka:
Utajiri haujengwi kwa kupata vitu vingi au kununua vitu vya bei kubwa. Unajengwa kwa kutambua thamani, kufanya maamuzi sahihi na kutumia fedha katika mambo yanayozalisha manufaa yanayolingana na gharama zake.
Kabla ya kutumia fedha, si sahihi kuangalia bei pekee, kwamba “Hiki kinauzwa kwa bei gani?” Jiulize pia, “Nitapata thamani gani kutokana na fedha nitakazotumia kwenye hiki?”
Karibu kundini kwa makala na vitabu 👇
https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?s=cl&p=a&mlu=0
13/10/2026
KANUNI YA 15: FEDHA NA FURAHA — ELEWA UHUSIANO WAKE
Fedha na furaha ni vitu viwili tofauti
Kuna mambo mengi yanayoweza kutufanya tusiwe na furaha, k**a vile kuondokewa na mtu wa karibu, kupoteza kazi au kuugua...
Lakini pia kuna baadhi ya mambo yanayohusiana na fedha, namna tunavyozipata na namna tunavyozitumia yanaweza kutupotezea furaha
Mfano:
- Kuwa na fedha nyingi kupita kiasi
- Kupungukiwa na fedha
- Kuwa na vitu vingi kupita kiasi
- Kutokuwa na vitu vya kutosha
Jambo muhimu tunalopaswa kulielewa ni kwamba fedha na furaha si lazima viwe kitu kimoja.
Fedha haitoi uhakika wa moja kwa moja katika kuwa na furaha.
Ndio maana unaweza kuwa na furaha katikati ya umaskini, ukawa na furaha katikati ya utajiri. Vilevile, unaweza kuwa maskini au tajiri asiye na furaha.
Unaweza kujiwekea matarajio mengi juu ya fedha na bado ukavunjika moyo unapozipata kutokana na namna zinavyoweza kuwa na ukomo katika baadhi ya mambo.
Huenda ukauliza, kanuni hii inatutaka tufanye nini hasa?
Jibu ni hili: Usitarajie mengi kupita kiasi kutokana na fedha.
Cha kujifunza katika kanuni ya 15
1. Fedha na furaha ni vitu viwili tofauti
Richard Templar anatufundisha kutofautisha kati ya kuwa na uwezo wa kifedha na kuwa na furaha maishani.
Fedha zinaweza kutuwezesha kupata chakula bora, makazi mazuri, huduma za afya, elimu na mazingira yenye usalama zaidi. Zinaweza kupunguza matatizo mengi yanayotokana na ukosefu wa mahitaji muhimu.
Hata hivyo, hazituhakikishii upendo, amani ya moyo, uhusiano mzuri na watu wengine au kuridhika na maisha.
Mtu anaweza kuwa na mali nyingi lakini akakosa amani. Vilevile, mtu mwenye kipato cha kawaida anaweza kufurahia maisha yake kwa sababu ana afya, mahusiano mazuri na malengo yenye maana.
2. Usitumie fedha kufidia mapungufu ya ndani
Baadhi ya watu hununua vitu vya gharama kubwa ili waonekane wa muhimu, wenye mafanikio au wakubalike katika jamii.
Hili huwa ni tatizo maana mtu huamua thamani yake ipimwe katika vitu na sio utu, kusudi na uwezo wa ndani ambapo vitu hivyo vinaweza kuchakaa, kupita ama kutokuchukuliwa katika thamani ileile na kila mtu hivyo humvunja moyo.
3. Furaha katika fedha inategemea mazingira na mtazamo.
Ukiwa huna fedha za chakula, malazi au matibabu, kupata fedha kunaweza kuboresha maisha yako kwa kiasi kikubwa. Katika mazingira hayo, fedha zina mchango wa moja kwa moja katika ustawi na furaha yako.
Lakini ikiwa una fedha nyingi na chanzo cha huzuni yako ni upweke, migogoro ya kifamilia, kutoridhika na maisha au kukosa kusudi, fedha huenda zisitatue matatizo hayo.
Kwa hiyo, tafuta ukwasi kwa bidii, utumie kwa busara na ufurahie matunda yake. Lakini usiweke furaha yako yote katika kile unachotarajia kukipata kutokana na fedha.
Usisubiri uwe tajiri ndipo ujifunze kuwa na furaha. Furaha si jambo la kusubiri, ni jambo la kuliishi kila siku bila kujali hali.
Karibu kundini kwa makala na vitabu;
https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?s=cl&p=a&mlu=0
12/10/2026
KANUNI YA 14: USITAFUTE FEDHA KWA KUTENDA MAOVU
The Rules of Wealth (Kanuni za Ukwasi) — Richard Templar
Ninapenda kauli mbiu ya Google isemayo, “Don't be evil" / Usiwe mwovu.” Kauli hii inaendana na jambo muhimu katika kutafuta ukwasi: usifanye maovu ili kupata fedha. Ikiwa ili kupata fedha zako ni lazima udanganye, uibe, uwahadae watu, uvunje sheria au utumie njia zisizo za haki, basi fedha hizo hazistahili maana si zao la gharama sahihi.
Kutafuta fedha kunapaswa kuwa jambo lililo katika misingi sahihi. Ikiwa hufurahii mafanikio yako kwa sababu ya namna ulivyoyapata, kuna haja ya kutafakari upya njia unayotumia.
Mwandishi anaeleza habari za mhalifu mkubwa aliyewahi kumfahamu. Mtu huyo alimweleza kuwa hapana uzuri wowote katika kutokuwa mnyoofu.
Maisha ya uhalifu hayakuwa na uhuru kwa sababu ilimbidi awe mwangalifu sana ili asigundulike kiasi ambacho hangejiweka katika mazingira yoyote ambaye yangemleta karibu na polisi na hata kusababisha kufuatiliwa.
Alikuwa hajihusishi na sherehe za usiku, alijiepusha na; makosa madogomadogo, kumiliki vitu vya kifahari, kuishi maisha ya anasa kupita kiasi, kwa sababu mambo hayo yangeweza kumweka kwenye jicho la polisi. Hata kosa dogo la barabarani lingeweza kumletea matatizo.
Mfano huu unaonyesha namna mtu anavyoweza kujitengenezea maisha yenye vikwazo kwa sababu ya njia aliyoichagua kupata fedha. Badala ya fedha kumpa uhuru, zinakuwa sababu ya kuishi kwa tahadhari na hofu kubwa.
Lakini pana faida katika kuishi maisha masafi, unakuwa huru na hubebi hofu ya kuangukia hata katika makosa madogo.
Unakuwa na hisia ya kujiamini na amani ya moyo, maana unakuwa hujajenga mafanikio yako kwa kuwadanganya au kuwadhulumu wengine. Hiyo ni faida ambayo hata fedha haiwezi kuinunua.
Mtu anapolazimika kufanya maovu ili kupata fedha, hiyo ina maana ameshindwa kutafuta njia bora ya kufanikiwa, ni mvivu, ameshindwa kufikiri sawasawa, na hana ubunifu katika kutatua changamoto.
Ili kufanikiwa kwa njia halali, tunahitaji kuwa makini na matendo yetu na namna tunavyopata fedha.
Mambo ya Kuzingatia
1. Kubali mchakato, si njia za mkato. Ubunifu na fikra sahihi vinaweza kukusaidia kupata fedha bila kuvunja misingi ya uadilifu.
2. Jiulize k**a unaweza kujivunia moyoni mwako chanzo cha fedha zako.
3. Usivutiwe na utajiri wa mtu bila kuzingatia namna alivyoupata. Kuwa na fedha nyingi hakumaanishi kuwa kila alichofanya ili kuzipata ni sahihi.
Panaweza kuwa mifano mingi ya watu maarufu na matajiri waliopata fedha zao kwa kutenda maovu. Na ni kweli kwamba wana utajiri, lakini ukiwatazama machoni, unaona nini?
Je, wana amani, dhamiri zao zinawashuhudia nini?
Je, wanaaminika katika jamii, mahusiano yao yakoje?
Je! Unatamani maisha yao au ungependa kuishi kwa utulivu, ukijua kwamba ulipata fedha zako kwa njia halali, ya uaminifu na ya haki?
11/10/2026
KANUNI YA 13: UNAWEZA KUPATA FEDHA NYINGI, KUFURAHIA KAZI YAKO NA KULALA KWA AMANI USIKU
> You can make lots of money, you can enjoy your job, and you can sleep nights.
UCHAMBUZI WA KANUNI YA 13
Watu wengi huhusisha fedha na ukwasi na dhana potofu k**a vile;
- Ili kutengeneza fedha, ni lazima uwe mtu asiyejali wengine, mwenye hila na anayejali maslahi yake binafsi pekee.
- Kuwa na ukwasi kunamaanisha kuishia kwenye matatizo ya moyo, kukosa usingizi na matatizo mengine ya kiafya yanayotokana na msongo wa mawazo.
- Kutafuta fedha nyingi kunakwenda sambamba na ukatili, udanganyifu, uchoyo na kupoteza misingi ya maadili.
Hata hivyo, Richard Templar anaeleza kuwa mambo yanaweza kuwa hivyo kwa baadhi ya watu, lakini si lazima yawe hivyo. Na hayapaswi kuwa hivyo.
Uzuri wa fedha ni kwamba fursa za kuzipata zipo kwa kila mtu, k**a tulivyoona katika Kanuni ya 1 (Yeyote anaweza kuwa na ukwasi). Hivyo, si lazima mtu apoteze maadili ili aweze kupata fedha nyingi. Watu wengi wa kawaida, wenye utu na wanaojali wengine, wameweza kujenga ukwasi mkubwa bila kuacha misingi yao ya maisha.
Unaweza kupata fedha nyingi, kufurahia kazi yako na kulala kwa amani usiku. Unachohitaji ni kuamua kwamba hivyo ndivyo utakavyoishi, bila kujali vishawishi vinavyoweza kukufanya uache msimamo wako. Baada ya kufanya uamuzi huo, unapaswa kuusimamia.
Hupaswi kuweka fedha mbele ya mambo mengine yote ya maisha, kiasi cha kusahau thamani ya utu, upendo na furaha.
Mwandishi anaeleza kuwa yeye binafsi angependa kuwa na tabasamu la upendo hata k**a kufanya hivyo kungemgharimu kiasi kidogo cha fedha. Hataki kupoteza kicheko, furaha maisha na kuwa na muda wa kufanya mambo anayoyapenda kwa sababu tu ya kutafuta ukwasi.
Anasisitiza kwamba hataki fedha zimfanye awe na wasiwasi kuhusu kazi au kipato kila anapokwenda kulala. Hataki kuendeshwa na kazi kiasi cha kusahau watoto, familia na umuhimu wa kukaa nje na kufurahia mwanga wa jua mara kwa mara. Hataki pia kukosa muda wa kupumzika.
Kwa upande mwingine, anataka kupata fedha nyingi, kufurahia kazi yake na kuwa na amani ya moyo. Anachokataa ni kupoteza maadili yake, kutumia muda mchache kupita kiasi na familia yake au kupoteza furaha yake kwa ajili ya fedha.
Kwa hiyo, mwandishi anasisitiza kuwa inawezekana kuwa mtu mwenye maadili mema, mwenye furaha na mwenye ukwasi kwa wakati mmoja. Ingawa wakati mwingine inaweza kuonekana kana kwamba haiwezekani, ukweli ni kwamba inawezekana.
Lengo lake ni kuvunja dhana potofu zinazohusishwa na fedha na ukwasi.
MAFUNZO MUHIMU KUTOKANA NA KANUNI YA 13
1. Ukwasi haupaswi kukugharimu utu wako.
Kupata fedha nyingi hakumaanishi kwamba ni lazima uwe mdanganyifu, mkatili au mtu asiyejali maslahi ya wengine. Unaweza kufanikiwa kifedha huku ukiendelea kuwa mwaminifu na mwenye maadili mema.
2. Fedha ni sehemu ya maisha, si maisha yote.
Fedha zina thamani kwa sababu zinatuwezesha kupata mahitaji, kutimiza malengo na kuboresha maisha yetu. Hata hivyo, hazipaswi kuchukua nafasi ya familia, afya, furaha na mahusiano yenye maana.
3. Kazi inapaswa kuwa sehemu ya maisha yenye maana.
Ni vizuri kujituma na kutafuta kipato, lakini si busara kuruhusu kazi itawale maisha yako kiasi cha kukunyima muda wa kupumzika, kujenga mahusiano na kufurahia matunda ya juhudi zako.
4. Amua mapema mipaka ambayo hutavuka kwa ajili ya fedha.
Ikiwa uaminifu, familia na afya ni mambo muhimu kwako, yafanye kuwa sehemu ya maamuzi yako ya kifedha. Usisubiri mpaka upoteze mambo hayo ndipo uanze kutafakari kuhusu gharama ya kutafuta ukwasi.
5. Pima mafanikio kwa namna unavyoishi, si kwa kiasi cha fedha ulicho nacho pekee.
Mtu anaweza kuwa na fedha nyingi lakini akakosa amani, furaha na muda wa kufurahia maisha yake. Kwa hiyo, mafanikio yanapaswa kuzingatia pia ubora wa maisha, si ukubwa na wingi wa mali pekee.
Kujiunga na kundi la vitabu na makala;
https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?s=cl&p=a&mlu=0
10/10/2026
KANUNI YA 12: USIICHUKULIE FEDHA KUWA SULUHISHO LA KILA TATIZO
> Ukichukulia fedha kuwa suluhisho la kila kitu, huwa tatizo.
Mara nyingi, tunapokabiliwa na matatizo ya maisha, huwa tunafikiri kwamba k**a tungekuwa na pesa za kutosha, tungeweza kuyatatua yote. Mtu anaweza kuamini kwamba akipata kiasi fulani cha fedha, matatizo yake yatakwisha, atakuwa na furaha, atapata afya bora na mahusiano yake yatakuwa mazuri zaidi.
Lakini je, fedha ni jawabu la mambo yote? La!
Fedha inaweza kukuwezesha kupata huduma bora za afya, lakini haiwezi kukuhakikishia kutokuwa mgonjwa.
Inaweza kukuwezesha kununua chakula bora, lakini hilo pekee halikuhakikishii afya njema.
Inaweza kukuwezesha kuishi katika nyumba nzuri na kupata mahitaji mengi ya maisha, lakini haimaanishi kwamba utakuwa na furaha ya kudumu au maisha yenye amani.
Hata katika mahusiano, fedha haiwezi kukuhakikishia kwamba watu watakupenda kwa dhati, watakuheshimu au wataelewana nawe.
Fedha inaweza kupunguza baadhi ya migogoro inayotokana na ukosefu wa mahitaji, lakini haiwezi kuondoa matatizo yote yanayotokana na tabia, kutokuaminiana, mawasiliano mabaya, kutokuwajibika kutokuelewana na tofauti za mitazamo.
Mtego huwa ni kuamini na kuichukulia fedha k**a suluhisho la kila kitu. Hivyo kutumia muda mwingi kuitafuta huku wakati mwingine tukipuuza vyanzo halisi vya matatizo yetu.
Ni kawaida mtu kutafuta fedha akiamini ajapo ipata itasuluhisha na kumpatia vyote, halafu akishaipata bado inashindwa kumpatia na kumsuluhishia baadhi ya vitu.
Hii humfanya mtu kujifunza kwa japo kwa kuchelewa kuwa mambo yote ni ubatili tena ni kujilisha upepo ilihali angeweza kujifunza mapema.
Chukulia mtu anayeamini kwamba akipata utajiri atakuwa na furaha, ilhali tatizo lake linahitaji tu, kubadilisha mtazamo, tabia au namna anavyohusiana na wengine.
Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba fedha haina umuhimu. Fedha ni nyenzo muhimu inayoweza kutuwezesha kupata suluhisho, kupunguza ugumu wa maisha, na kukabiliana na changamoto nyingi.
Tofauti tu ni kwamba fedha haiwi jawabu kwa kila jambo.
Hivyo, fedha inaweza kurahisisha mambo mengi maishani, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya nidhamu, hekima, upendo na utatuzi sahihi wa matatizo.
Tunapaswa kujifunza kutofautisha kati ya matatizo yanayohitaji fedha na yale yanayohitaji mabadiliko ya fikra, tabia au maamuzi.
Tunapokabiliwa na changamoto, badala ya kujiuliza tu, “Nahitaji fedha kiasi gani ili kutatua hili?”, tunapaswa pia kujiuliza, “Tatizo hili linasababishwa na nini, na ni hatua gani inayoweza kulitatua kwa msingi wake?”
Kumbuka: Fedha si dhamana ya maisha yasiyo na matatizo, kwahiyo kule kutafuta fedha k**a jawabu pekee, kusiwe sababu ya matatizo mengine na upofu wa kutoona aina nyingine ya majawabu.
09/10/2026
KANUNI YA 11: KOKOTOA FAIDA HALISI
> CALCULATE THE NET RETURN
Kokotoa faida halisi kabla ya kufanya uamuzi.
Mara nyingi tunapoangalia fursa ya kifedha, tunavutiwa na namba tunayoiona mwanzoni. Tunaweza kuona kwamba uwekezaji fulani unatoa asilimia fulani ya faida na mara moja tukahitimisha kwamba ni uwekezaji mzuri.
Lakini kabla ya kufanya uamuzi, kuna swali muhimu zaidi la kujiuliza: baada ya kutoa gharama zote, kodi, gharama za endeshaji na gharama nyingine, ni kiasi gani hasa kitabaki?
Huo ndio umuhimu wa kuhesabu faida halisi.
Kwa mfano, unaweza kuona fursa ya uwekezaji inayotoa faida ya asilimia 30 na ukaona kwamba ni nzuri. Lakini k**a kuna gharama mbalimbali zinazohusika, faida hiyo inaweza kupungua kwa kiasi kikubwa.
Hili linaonyesha kwa nini ni hatari kuvutiwa na “namba ya juu” bila kuangalia kile kinachobaki baada ya gharama zote. Faida ya asilimia 30 kwenye karatasi si sawa na asilimia 30 katika uhalisia.
Kanuni hii pia inatukumbusha kwamba si kila ongezeko la thamani tunalotarajia kwenye uwekezaji linapaswa kuchukuliwa k**a faida ya uhakika. Kwa mfano, thamani ya nyumba inaweza kuongezeka baada ya miaka mitano au kumi, lakini hilo si jambo la uhakika. Thamani inaweza kuongezeka kwa kiwango cha chini tofauti na matarajio, kubaki katika kiwango kilekile au hata kushuka. Na unapouza, unaweza pia kukutana na gharama au kodi zinazopunguza kiasi utakachobaki nacho.
Kwa mtazamo mpana zaidi, kanuni hii inatufundisha kutofautisha kati ya faida inayoonekana na faida halisi. Katika fedha, namba ya mwanzo inaweza kuvutia, lakini namba muhimu zaidi ni ile inayobaki baada ya kila kitu kukamilika.
Hii inaweza kutumika katika maamuzi mengi ya maisha. Unapofikiria kununua nyumba, gari, kufanya uwekezaji, kwenda likizo au hata kuacha kazi, si muhimu tu kujiuliza, “Ninapata kiasi gani?” Bali pia, “Baada ya gharama zote, nitabaki na kiasi gani?”
Kwa sababu wakati mwingine jambo linaweza kuonekana kuwa zuri kwa kuangalia hesabu ghafi, lakini likawa si zuri sana unapofanya hesabu kamili.
Hivyo, kabla ya kusema kwamba fursa fulani ni nzuri, hesabu faida halisi. Usifanye uamuzi kwa kutegemea namba inayovutia macho mwanzoni; fanya uamuzi kwa kuangalia kile kitakachobaki baada ya gharama zote.
08/10/2026
KANUNI YA 10: ELEWA KWAMBA FEDHA HUZAA FEDHA
> MONEY MAKES MONEY. THE RICH GET RICHER.
Hapana ukweli mkuu k**a huu – fedha hutengeneza fedha.
Sehemu ya fedha inapowekwa mahali inapo weza kujizalisha, badala ya kutumika yote, huanza kumfanyia kazi mwenye nayo.
Wanaojenga ukwasi wamejifunza kutenganisha sehemu ya fedha wanayopata kwa ajili ya matumizi na sehemu nyingine kwa ajili ya kuzalisha fedha zaidi.
Kwa lugha ya mfano, ni k**a kufuga sungura. Ukipata sungura wachache halafu ukawachinja na kuwala wote, utabaki bila sungura. Lakini ukiwaacha baadhi yao wazaliane, idadi yao itaongezeka. Baadhi unaweza kuwauza au kuwatumia k**a kitoweo, huku wengine wakibaki kwa ajili ya kuzaliana zaidi.
Ndivyo ilivyo kwa fedha pia.
Ukitumia kila unachopata, kanuni ya fedha kuzaa fedha haiwezi kufanya kazi. Lazima kuwe na sehemu ya mapato inayotengwa kwa ajili ya “kuzalisha”— kuwekezwa, kutumika k**a mtaji au kuwekwa kwenye mali inayoweza kuzalisha mapato zaidi.
KINACHOWAKWAMISHA WENGI
Fedha si tatizo kwa sababu karibia kila mtu hupata fedha, iwe ni kwa kiasi kidogo au kwa wingi, kwa kupewa ama kwa kutafuta mwenyewe.
Kinachowatesa watu wengi ni spending mentality–mtazamo wa kutumia tu.
Na kiuhalisia matumizi hayana ukomo hata k**a ungepewa kiasi kingi unachoweza kudhani kitakidhi, k**a una tabia ya kutumia tu, utatumia chote.
Hili linathibitika kisaikolojia kwa sababu ya _lifestyle creep_—mfumuko wa matumizi kulingana na ongezeko la kipato.
Tabia hii ndio hufanya watu wengi waifanyie kazi pesa mpaka pindi nguvu zinapowaisha (uzee) pasina kufikia uhuru wa kifedha.
Chukulia mtu anayelipwa mshahara–halafu fedha inaishia kwenye kodi, chakula, mavazi, starehe, madeni, misaada, na mahitaji mengine halafu mwezi unaisha. Mwezi unaofuata mchakato unakuwa uleule, mtu wa aina hii hawezi kujenga ukwasi.
MAWAZO MUTAMBUKA: UHALISIA WA FEDHA KUZAA FEDHA
Katika moja ya podcast za Let's Impact Millions, ilijengwa hoja kuhusu uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja hasa UTT AMIS, nikimnukuu msemaji:
"Kitendo cha kuwa kijana UTT haikufai"..."k**a una miaka 30 kuendelea 👍🏽, chini ya hapo achana nayo..."
Msemaji hoja yake ilikuwa kwamba vijana wanapaswa kuwa tayari kuchukua hatari ili waweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa zaidi matinki ikiwa ileile "fedha kuzalisha fedha, badala ya kujifunga katika maisha ya kutafuta usalama wa kipato kidogo.
Kwamba walimu wa biashara wafundishe vijana elimu ya biashara zaidi— kujenga na kukuza biashara kuliko uwekezaji wa pamoja.
Dhima ya hoja hiyo ni nzuri. Hakika, katika kujenga ukwasi mkubwa, kuna wakati mtu anahitaji kuwa tayari kuchukua hatari zilizopimwa (calculated risks), kujaribu fursa mpya na kutafuta namna ya kuongeza uwezo wake wa kuzalisha.
Lakini kuna jambo moja ambalo hatuwezi kulifunikia kombe uhalisia wake kwa kule kusema tujikite na baishara zaidi.
Dhima ya kanuni hii ni mtu kutenga sehemu ya kiasi anachopata hata k**a ni kidogo na kukiweka mahali kinapoweza kuzaa, ambapo mifuko ya pamoja ya uwekezaji ni eneo moja wapo.
Hatuwezi kubeza uwekaji wa sehemu ya kipato hata ikiwa ni ndogo kwenye mifuko hiyo kwa sababu ya;
Mosi, –tabia inayozalishwa na kitendo hicho kinaporudiwarudiwa.
Tabia ya kuweka akiba hufuta mtazamo wa kutumia tu, na kuleta udhibiti wa matumizi.
Pili, –faidi ya muda, siku zote ukubwa wa matokeo ya tabia huendana na muda.
Tabia inayojengwa mapema faida yake hujilimbikiza zaidi na muda, kwa hiyo huwezi kusema utasubiri uwe na miaka 30 ndio uanze kuweka akiba au kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja.
Warren Buffett ni mmoja wa wawekezaji mashuhuri zaidi duniani katika hisa, na historia yake ni mfano mkubwa wa jinsi muda, uwekezaji wa muda mrefu na riba inayojilimbikiza (compound interest) vinavyoweza kujenga ukwasi, Buffett alianza kuwekeza akiwa na miaka 11, wala hakusubiri afikie miaka 30.
Ndiyo maana muda ni sehemu muhimu sana katika kujenga tabia na ukwasi.
Usisubiri upate fedha nyingi ndipo uanze kuweka akiba ya uwekezaji. Jenga kwanza tabia; ili ukipata fedha nyingi, tabia hiyo ziikute.
Kumbuka:
> Ni rahisi kutumia kinachobaki baada ya kuweka akiba, lakini ni vigumu kuweka akiba kinachobaki baada ya matumizi.
MWENYE NACHO HUONGEZEWA
Matajiri huzidi kuwa matajiri na maskini kuwa maskini. Kilicho nyuma ya kauli hii ni kanuni.
Anayetenga sehemu ya anachopata k**a akiba atakitumia k**a;
Mtaji ambao anaweza kuuwekeza;
Uwekezaji unazalisha faida (riba).
Faida (riba) anaweza kuiongeza kwenye mtaji ili kuukuza.
Mtaji unaokuzwa unazalisha faida zaidi.
Faida zaidi inaweza kurejeshwa tena kwenye mtaji....mzunguko unaenda hivyo
Ambao unakuwa mzunguko wa ukuaji.
Pia akiba hiyo anaweza kuitumia kujikwamua na dharura badala ya kulazimika kuingia kwenye madeni.
...hapa mwenye nacho anaongezewa.
Kwa upande mwingine, mtu asiyeweka akiba atalazimika kutumia karibu kila anachopata ili kukidhi mahitaji yake. Kwa hiyo, hakuna sehemu inayobaki ya kuanza kuzalisha fedha.
Na zinapotokea dharura atalazimika kukopa kujinusuru.
...hapa asiyenacho, hata kile kidogo alichonacho kinapotea.
KINACHOPUNGUA KWENYE MAARIFA YAKO
Huenda mimi sio wa kwanza kukuandikia haya.
Unajua unapaswa kuweka akiba lakini huweki.
Unajua unapaswa kuacha matumizi mabaya lakini bado hujaacha.
Unajua unapaswa kuwekeza lakini huwekezi.
Shida yako sio maarifa maana unafahamu, bali ni nidhamu ya kufanyia kazi maarifa, kwahiyo jenga nidhamu.
Karibu kundini:
https://chat.whatsapp.com/HMG6yjovJrSAm99koqx8Og?s=cl&p=a&mlu=0
Click here to claim your Sponsored Listing.
Website
Address
Dar Es Salaam
Alerts
Be the first to know and let us send you an email when Maskani ya Vitabu na Maarifa posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.